Kila mtu ana msimbo wa kijenetiki anaoirithi kutoka kwa kila mmoja wa wazazi wake. Msimbo huu unaundwa na vipengele vya taarifa vinavyobeba maelekezo ambayo mwili unahitaji ili kufanya kazi ipasavyo.
Sehemu kubwa ya msimbo wa kijenetiki huwa sawa kati ya watu mbalimbali. Hata hivyo, tofauti katika msimbo huu wa kijenetiki huitwa tofauti za kijenetiki.
Tofauti za kijenetiki huchangia sifa zinazotufanya kuwa wa kipekee kama vile rangi ya macho, urefu, na mapendeleo ya ladha.
Tofauti za kijenetiki zinaweza pia kuathiri hatari yetu ya kupata magonjwa fulani — hizi huitwa tofauti zenye hatari.
Ili kugundua tofauti zenye hatari, wanasayansi hulinganisha misimbo ya kijenetiki ya watu wasio na ugonjwa na wale walio na ugonjwa.
Ikiwa tofauti ya kijenetiki inatokea mara nyingi zaidi kwa watu wenye ugonjwa, huwa inahusishwa na kuongezeka kwa hatari.
Ikiwa tofauti ya kijenetiki inatokea mara nyingi zaidi kwa watu wasio na ugonjwa, huwa inahusishwa na kupungua kwa hatari.
Tofauti zenye hatari za kijenetiki zinaweza kuongeza au kupunguza hatari ya mtu kuugua ugonjwa, na kila moja inaweza kuwa na kiwango tofauti cha athari.
Baadhi ya tofauti zenye hatari za kijenetiki zina athari kubwa kwa hatari ya ugonjwa, na baadhi zina athari ndogo.
Tofauti moja ya kijenetiki huenda ikaathiri kwa kiwango kidogo , lakini tofauti nyingi kama hizo kwa pamoja zinaweza kuwa na athari kubwa zaidi.
Ili kuhesabu alama ya jeni nyingi ya mtu kwa ugonjwa fulani, wanasayansi hujumlisha tofauti za kijenetiki zinazoongeza na kupunguza hatari, pamoja na uzito wa athari zake.
Alama ya jeni nyingi huonyesha jinsi hatari yako ya kupata ugonjwa inavyolingana na hatari ya watu wengine.
Wanasayansi wanaweza kuhesabu alama ya jeni nyingi kwa idadi yote ya watu katika jamii.
Baadhi ya watu watakuwa na alama ya juu au ya chini, kutegemea na idadi ya tofauti za kijenetiki zinazoongeza au kupunguza hatari, pamoja na kiwango cha athari cha kila tofauti.
Watu wenye idadi takriban sawa ya tofauti za kijenetiki zinazoongeza na kupunguza hatari huwa na hatari ya wastani ya ugonjwa kulingana na jenetiki zao.
Watu wenye tofauti nyingi zaidi za kijenetiki zinazoongeza hatari huwa na hatari kubwa ya kupata ugonjwa kulingana na jenetiki zao.
Watu wenye tofauti nyingi zaidi za kijenetiki zinazopunguza hatari huwa na hatari ya chini ya kupata ugonjwa kulingana na jenetiki zao.
Idadi kubwa ya watu wana hatari wastani ya ugonjwa kulingana na jenetiki zao.
Alama yako inaweza kuwa juu kuliko wastani, kumaanisha kuwa una hatari kubwa ya kijenetiki ya kupata ugonjwa ikilinganishwa na idadi kubwa ya watu.
Iwapo alama yako ya jeni nyingi iko katika asilimia ya 95, haimaanishi kuwa una uwezekano wa asilimia 95 wa kupata ugonjwa. Badala yake, inamaanisha kwamba — kati ya watu 100 — alama yako iko juu kuliko ya watu 95, na sawa na au chini ya watu 5.
Alama yako inaweza kuwa chini kuliko wastani, kumaanisha kuwa una hatari ndogo ya kijenetiki ya kupata ugonjwa ikilinganishwa na idadi kubwa ya watu.
Iwapo alama yako ya jeni nyingi iko katika asilimia ya 5, haimaanishi kuwa una uwezekano wa asilimia 5 wa kupata ugonjwa. Badala yake, inamaanisha kwamba — kati ya watu 100 — alama yako iko juu kuliko ya watu 5, na sawa na au chini ya watu 95.
Alama ya jeni nyingi kwa ugonjwa wa mishipa ya moyo (coronary artery disease) inategemea tu msimbo wa kijenetiki uliozaliwa nao.
Ingawa huwezi kubadilisha alama yako ya jeni nyingi, kuzingatia mtindo bora wa maisha na kushirikiana na wataalamu wa afya kutibu vihatarishi vya kiafya kunaweza kupunguza hatari yako kwa kiasi kikubwa.
Shirika la Moyo la Marekani (American Heart Association) limeainisha mambo saba muhimu yanayochangia afya bora ya moyo (‘Life’s Simple 7’). Watu wenye angalau mambo matano kati ya hayo saba hupunguza hatari ya kufa kutokana na maradhi ya moyo kwa asilimia 78 , ikilinganishwa na wale wasiotimiza hata moja kati ya mambo hayo ya kiafya.
Una Shinikizo la damu la kawaida ni lile lenye kipimo cha juu (systolic) chini ya 120 mm Hg na kipimo cha chini (diastolic) chini ya 80 mm Hg.
Ikilinganishwa na wale walio na shinikizo la damu lililoongezeka, watu wenye shinikizo la damu la kawaida wana hatari ya chini kwa asilimia 24* ya kupata ugonjwa wa mishipa ya moyo.
Kiwango cha kawaida cha cholesterol kwa watu wazima (bila matibabu) ni chini ya 200 mg/dl. Ikilinganishwa na watu wenye kiwango cha juu cha cholesterol, watu wenye cholesterol ya kawaida wana hatari ya chini kwa asilimia 16* ya kupata ugonjwa wa mishipa ya moyo.
Kiwango cha kawaida cha sukari kwenye damu (baada ya kufunga) ni chini ya 100 mg/dl. Ikilinganishwa na watu wenye kiwango cha juu cha sukari, watu wenye sukari ya kawaida wana hatari ya chini kwa asilimia 31* ya kupata ugonjwa wa mishipa ya moyo.
Mapendekezo ya sasa ya mazoezi yanashauri angalau dakika 150 kwa wiki za mazoezi ya kiwango cha kati, au dakika 75 kwa wiki za mazoezi ya kiwango cha juu, au mchanganyiko wa yote mawili.
Ikilinganishwa na wale wasiofanya mazoezi, watu wanaozingatia pendekezo hili wana hatari ya chini kwa asilimia 16* ya kupata ugonjwa wa mishipa ya moyo.
Lishe bora ina kiasi kikubwa cha vyakula vyenye afya kwa moyo — matunda, mboga, samaki, na nafaka zisizokobolewa — na kiasi kidogo cha vyakula visivyo na afya — chumvi nyingi na vinywaji vyenye sukari.
Ikilinganishwa na wale wenye mtindo wa lishe usiofaa, watu wanaofuata lishe bora wana hatari ya chini kwa asilimia 27* ya kupata ugonjwa wa mishipa ya moyo.
Uzito wa kawaida hufafanuliwa kama uwiano wa uzito na urefu wa mwili (BMI) chini ya 25 kg/m2. Ikilinganishwa na wale walio na kipimo cha juu cha BMI, watu wenye uzito wa kawaida wana hatari ya chini kwa asilimia 36* ya kupata ugonjwa wa mishipa ya moyo.
Kuvuta sigara ni mojawapo ya sababu kuu zinazoweza kuepukika za ugonjwa wa mishipa ya moyo. Ikilinganishwa na wale waliowahi kuvuta sigara, watu ambao hawajawahi kuvuta sigara wana hatari ya chini kwa asilimia 26* ya kupata ugonjwa wa mishipa ya moyo.